Mkoa wa Simiyu umejipanga kuandaa mwongozo wa uwekezaji kwa kila Kijiji na Mtaa utakaobainisha fursa za uwekezaji zilizopo katika kijiji na mtaa husika katika vijiji vyote 471 na Mitaa 92 ya wilaya zote tano za Mkoa huu, ikiwa ni maandalizi ya utekelezaji wa Falsafa ya Bidhaa Moja Kijiji Kimoja(OVOP) mwaka 2019/2020.
Hayo yamebainishwa Mjini Bariadi katika kongamano la kuwajengea uwezo Watendaji wa Vijiji 471, Watendaji wa Mitaa 92, Watendaji wa Kata 130 na Maafisa tarafa 16 juu ya kuibua fursa za uwekezaji kwa ajili ya kuandaa mwongozo wa uwekezaji kwa kila kijiji na mtaa, kwa kushirikiana na Wataalam kutoka Taasisi ya Utafiti wa Masuala ya Kiuchumi na Kijamii (ESRF), ambalo pia limewahusisha viongozi na watendaji wa Chama na Serikali ngazi ya wilaya na Mkoa.
Awali akifungua kongamano hilo Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema Mkoa huu unatekeleza Falsafa ya Bidhaa Moja Wilaya ambayo ilianza baada ya ESRF kufanya utafiti na kuibua fursa 26 ndani ya mkoa na sasa inajipanga kuandaa mwongozo wa uwekezaji kwa kila kijiji na kuanza utekelezaji wa Bidhaa Moja Kijiji Kimoja.
“Miaka mitatu ya utekelezaji wa Bidhaa Moja Wilaya Moja imetosha, mwaka 2019/2020 ni Bidhaa Moja Kijiji Kimoja, ESRF watatusaidia kufanya utafiti utakaoonesha kila kijiji kina fursa gani; Mkoa wa Simiyu utakuwa mkoa wa kwanza kwenye nchi hii ambao kila kijiji na mtaa utakuwa na mwongozo unaoonesha fursa za uwekezaji za kijiji au mtaa huo” alisisitiza.
Comments
Post a Comment