mahakama kuu ya mafisadi yamuhukumu Anna Chissano kifungo cha maisha

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi imemhukumu Raia wa Msubiji, Ana Moisie Chissano (36) kwenda jela kutumikia kifungo cha maisha baada yakukutwa na Kilo 3.03 za dawa za kulevya aina ya cocaine Hydrochloride.

Hukumu hiyo imesomwa leo katika mahakama hiyo iliyoketi chini ya Jaji Lilian Mashaka baada upande wa mashtaka kuthibitisha makosa bila kuacha shaka.

"Mahakama hii baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi sita wa Jamhuri kuthibitisha makosa dhidi yake, Mahakama yangu inakuhukumu kwenda jela kutumikia kifungo cha maisha kwa kosa la kukutwa na dawa hizo " amesema Jaji Mashaka.

Pia, Mahakama hiyo imeamuru dawa hizo za kulevya kuteketezwa kwa utaratibu unaostahili.

Akifafanua hukumu hiyo jaji alisema anatoa adhabu hiyo chini ya kifungu cha sheria namba 15 kidogo cha (1) (b) cha Sheria namba 5 ya 2015 ya kuzuia na kupambana na dawa za kulevya.

Jaji Mashaka amesema sheria hiyo inaelekeza mtu yoyote anayejihusisha na dawa za kulevya anapopatikana na hatia anapaswa kutumikia kifungo cha maisha jela.

Amesema mahakama yake imezingatia sheria ambayo imeweka adhabu kwa mtu kupitia kifungu hicho inayosema mtu yeyote atakayepatikana na hatia kwa makosa ya dawa za kulevya basi adhabu yake ni jela maisha.

Pia amesema dawa za kulevya ni tatizo linaloikabili jamii hivyo kwa njia yoyote yanapaswa kuzuiwa na jitihada za pamoja zinatakiwa zitekelezwe ili kupunguza tatizo ikiwemo kuwaadhibu wote wanaojihusisha na dawa za kulevya.

Kabla ya kutolewa adhabu, Jaji Lilian aliuliza upande wa mashitaka kama wanakumbukumbu zozote juu ya mshtakia, wakili Kakula alidai hawana kumbukumbu ya makosa lakini makosa hayo yamekuwa yakiongezeka na kusababisha kupotea kwa nguvu kazi kutokana na kutumia dawa za kulevya.

Comments